VIRUSI VYA HUMAN PAPILLOMA (HPV)

VIRUSI VYA HUMAN PAPILLOMA (HPV) NA ATHARI ZAKE

HPV ni aina ya virusi vinavyojulikana sana ambavyo vinaweza kusambazwa kiurahisi kwa njia ya kujamiiana. Virusi hivi vinaweza kusababisha matatizo mbali mbali ya afya kwa binadamu ikiwemo WARTS mpaka SARATANI.

Virusi hivi vipo vya aina nyingi sana ila kwa ujumla wake vimewekwa katika makundi makuu mawili;

  1. Virusi ambavyo sio hatarishi
  2. Virusi ambavyo ni hatarishi sana

Virusi ambavyo sio hatarishi ni vile ambavyo haviwezi kusababisha matatizo makubwa kama saratani na vile ambavyo ndio hatarishi zaidi vinaweza sababisha saratani. Maeneo ya mwili ambayo yanaweza kuonyesha kwamba umeshawahi kukumbana na virusi hivi ni kama ngozi ya mwilini pamoja na maeneo ya nje au ndani ya sehemu za siri kwa mwanaume na mwanamke.

Picha zifuatazo zinaonyesha dalili ya mtu ambaye ameshawahi kukumbana na virusi hivi:

Virusi vya HPV ambavyo ni hatarishi zaidi vinaweza kusababisha saratani katika maeneo kama uume, shingo ya mfuko wa kizazi, sehemu ya haja kubwa na kwenye koo. Lakini ni vyema kukumbuka kwamba watu wengi wenye virusi hivi wanakuwa hawana dalili yoyote na mda mwingine kama umeshaanza kuonyesha dalili basi unaweza kukuta kinga ya mwili inaweza kupambana na hali hiyo na kisha kuondoa tatizo hilo.

Kutokana na uhalisia kwamba virusi hivi havina tiba na ni rahisi sana kuvipata kwa wale ambao wameshaanza kujihusisha na maswala ya ngono, basi njia sahihi ya kujikinga ni kutumia condom na kuepuka ngono kwa njia ya mdomo. Zipo chanjo zinazoweza kutolewa kwa ajili ya kinga ila ni maalumu kwa wale wenye umri kati ya miaka 9-14. Hii inamaana kwamba kama umri wako upo juu zaidi ni vyema sana kufuatilia afya yako kama nitakavyoelekeza.

Miongozo ya kinga inatuelekeza kwamba ni vyema kwa mwanamke kufanya uchunguzi wa saratani (PAP TEST) ya shingo ya kizazi kila baada ya miaka 3 kama umri wako upo kati ya miaka 21-29. Unapofika miaka kati ya 30-65 unaweza kufanya uchunguzi huu pamoja na kuvipima virusi vyenyewe (HPV-DNA detection) kila baada ya miaka mitano . Na kama umri wako upo juu ya miaka 65 na haujawahi kupatikana na virusi hivi basi utakuwa hauna haja tena ya kuendelea na uchunguzi. Ila kama umeshawahi kuwa na dalili za virusi hivi au ulikutwa unavyo baada ya kupima, ni vyema kuendelea kufuatilia afya yako (ACOG).

 

Hitimisho:

Ni vyema kuhakikisha unapeleka watoto kupata chanjo na pia kama mzazi epuka ngono zembe. Kwa upande wa wanawake, hakikisheni mnafanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi. Na kwa upande wa wanaume wanao fanya ngono na wanaume wenzao pia ni vyema kuhakikisha unafanyiwa uchunguzi sehemu za haja kubwa. Nenda kwenye kituo cha afya kilichopo karibu yako kwa maelezo zaidi. Kinga ni bora kuliko tiba.

Share na Wengine

1 thought on “VIRUSI VYA HUMAN PAPILLOMA (HPV)”

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Appointment

Make appointment here