Umuhimu wa madini chuma kwa mama mjamzito

UMUHIMU WA MADINI CHUMA KWA MAMA MJAMZITO

Utangulizi

Madini ya chuma ni madini muhimu sana kwa mama wajawazito na wale ambao wanatarajia kuwa wajawazito. Tafiti zinaonyesha kwamba duniani, asilimia 37% ya wajawazito wana upungufu wa damu na asilimia 40% ya wajawazito hao upungufu wa damu unasababishwa na upungufu wa madini ya chuma (WHO). Tatizo hili linaonekana zaidi kwa nchi za afrika ikiwemo Tanzania ambapo tafiti zinaonyesha asilimia 57% ya upungufu wa damu kwa wajawazito zaidi inatokana na ukosefu wa madini ya chuma mwilini (Sunguya et al 2021).

Vyanzo vya madini chuma

Madini ya chuma yana vyanzo vingi mfano;

  • Jamii ya mboga za majani kama mchicha nk
  • Nyama kama ya ng’ombe, mbuzi nk
  • Vitu vya baharini kama dagaa, Samaki wa jodari, sangara nk
  • Matunda ingawa ni kwa kiwango kidogo mfano Mapera, mabungo, ndizi, parachichi nk

Ingawa madini ya chuma yanavyanzo vingi, sio kila mama ambaye ni mja mzito anaweza kupendelea kutumia vyanzo hivi. Wakati mwingine, kutokana na mahitaji ya madini haya kuongezeka mwilini kipindi cha ujauzito, sio rahisi kula vyakula hivi kwa kiwango kinacho takiwa. Hivyo, ili kurudisha madini haya mwilini kwa kiwango kinacho hitajika wahudumu wa afya wamekuwa wakitoa vidonge ambavyo ni mahususi kwa ajili ya kurudisha madini ya chuma.

Dalili za upungufu wa madini chuma kwa mama mjamzito:

  1. Kujisikia kuchoka na kukosa nguvu kuliko kawaida: hii inasababishwa na upungufu wa hewa safi (oxygen) kwenye misuli ya mwili.
  2. Ngozi ya mwili kuwa nyeupe, hii inajionyesha zaidi maeneo ya mikono, kucha, soli za miguu na hata macho.
  3. Kuhisi kukosa pumzi hata kwenye kazi nyepesi, hii ni kutokana na kiwango kidogo cha Oxygen kwenye damu.
  4. Kizunguzungu: unaweza hisi kama unataka kupoteza fahamu na hujitokeza unaposimama ghafla.
  5. Maumivu ya kichwa ya mara kwa mara: hii zaidi hujitokeza endapo oxygen haifiki vya kutosha kwenye ubongo
  6. Mapigo ya moyo kwenda kasi: Hii inatokea kwasababu moyo unahitaji kusukuma damu kwa haraka ili iweze kufanikisha kusafirisha kiwango kidogo cha Oxygen kilichopo  kwenye damu kifike kwenye viungo mbali mbali vya mwili kwa haraka.
  7. Kuwa na hamu ya vitu vya ajabu kama udongo, mchele, mkaa nk.
  8. Kuwa na uwezo mdogo wa kufikiria jambo: hii husababishwa na upungufu wa hewa safi (oxygen) kwenye ubongo.
  9. Kushuka kwa kinga ya mwili: hii itasababisha mwili wako kuwa katika nafasi ya kupata maambukizi mbali mbali yanaweza kuwa ya fangasi, bakteria au virusi.

Changamoto zinazoweza kujitokeza kwa mtoto kama mama anaupungufu wa madini chuma:

  1. Mtoto anaweza kuzaliwa na uzito mdogo kuliko kawaida
  2. Mama anaweza kujifungua kabla ya wakati, na watoto hawa wanakuwa na nafasi kubwa ya kupata shida ya mfumo wa hewa, chakula na ukuaji hafifu.
  3. Ukuaji wa mtoto ndani ya tumbo ulio hafifu (intrauterine growth restriction)
  4. Watoto wanaweza kupata upungufu wa damu kutokana na mazingira waliyokulia.
  5. Kinga ya mwili iliyo dhaifu. Hii itamweka mtoto kwenye hatarishi ya kupata magonjwa mbali mbali.

Maelezo haya yanaonyesha kwamba ni muhimu sana kwa mama mjamzito kuwa na kiwango kizuri sana cha madini chuma kwa ajili yake binafsi na mtoto anayekuwa tumboni. Kuhudhuria  kliniki mara kwa mara, kuzingatia lishe na kufuata ushauri wa watoa huduma za afya juu ya matumizi ya madini chuma yataweza kupunguza nafasi ya kupata changamoto zilizo ainishwa hapo juu.

Hitimisho:

Ni vyema kupata ushauri na kujua afya yako kabla hujafanya maauzi ya kubeba mimba. Kinga ni bora kuliko tiba.

Share na Wengine

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Appointment

Make appointment here