Umuhimu wa FOLIC ACID kabla na wakati wa Ujauzito

Ujauzito ni kipindi ambacho mwanamke anakuwa na hali ya mabadiliko yanayotokana na kiumbe ambacho kinakuwa ndani ya mji wa mimba. Na kitaalamu, ujauzito ni swala ambalo linahitaji mipango ili kuhakikisha safari ya mwanamke ambaye amepata mimba hiyo haina misukosuko na hata kama itakuwepo basi alishapewa fununu zake hapo awali. Mipango ambayo inatakiwa kupangwa ni kama ifuatayo:

  1. Kukaa mme na mke na kuzungumza mda gani ambao kwenu utakuwa sahihi wa kupata ujauzito. Baadhi ya wanandoa (couples) wanakuwa hawapo tayari kwani wengi wao wanasoma au wanakuwa wapo katika wakati mgumu wa kiuchumi. Kwa mantiki hiyo kama wanafamilia hamjalizungumza hili kitakachotokea ni kuingia kwenye msongo wa mawazo na kisha kuona safari ya ujauzito ni ngumu sana kwa sababu hamkupanga hapo awali.
  2. Kuonana na daktari na kuweza kumshirikisha mipango yenu ya kutaka kupata mtoto/Watoto. Hili swala la kumwona daktari kabla ya kubeba mimba limekuwa ni kitendawili. Kilicho zoeleka ni kupata mimba kisha kwenda kuonana na daktari kwa ushauri. Manufaa ya kuonana na daktari kabla ya kubeba mimba ni mengi sana. Mfano: kufanyiwa uchunguzi kama unamagonjwa yasiyo ambukizwa; shinikizo la damu, kisukari, seli mundu (sickle cell), uvimbe kwenye mji wa mimba (uterine fibroid), saratani za shingo ya kizazi n.k. Pamoja na hayo, utapata nafasi ya kufanya vipimo kuweza kuona kama kuna magonjwa yanayo ambukizwa mfano; kaswende, ukimwi n.k. Kama kunatatizo litakalo gundulika na linahitaji kupatiwa tiba kabla ya kupata mimba, basi daktari husika atafanya hivyo. Kama hamna tatizo la kiafya lilio onekana basi daktari pia atachukua nafasi hiyo ya kukupa maelezo juu ya mambo yatakayoweza kujitokeza kipindi cha ujauzito. Na mwisho kabisa, daktari atakupa dawa za kuandaa mwili wako kuwa tayari kubeba mimba ili kuongeza nafasi ya kupata mtoto asiye na matatizo ya mfumo wa fahamu.

Hivyo, katika mipango hiyo, dawa ambayo ni ya msingi na sio ya kuikosa ni FOLIC ACID. Dawa hii imethibitishwa kuwa inauwezo wa kusababisha kuwe na ukamilifu mzuri wa uumbwaji wa mfumo wa fahamu wa mtoto. Matatizo yanayoweza kuzuiwa kwa kutumia dawa hizi ni kama inavyoonekana kwenye picha za hapo juu.

Baadhi ya vyakula vinavyoweza kukupatia folate/folic acid; mboga za majani (spinach), Maharagwe, karanga, matunda, mayai, maini na vyakula vya baharini. Jambo kubwa la kuzingatia ni kwamba, folic acid inayotengenezwa (iliyopo kwenye mfumo wa vidonge) inaweza kunyonywa kiurahisi na mfumo wa chakula kuliko ile inayopatikana kwenye vyakula. Ndio maana inasisitizwa zaidi kutumia folic ya vidonge kuliko kutegemea ya kwenye chakula peke yake.

Hitimisho: Upo umuhimu wa kuonana na daktari kabla ya kuamua kubeba mimba na pia hakikisha unatumia folic acid kuanzia miezi 2-3 kabla ya kubeba mimba. Tukumbuke kwamba kinga ni bora kuliko tiba.

Share na Wengine

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Appointment

Make appointment here