MYOMECTOMY (UPASUAJI WA KUTOA UVIME UITWAO MYOMA AU UTERINE FIBROID)

Nini maana ya myomectomy?

Hii ni aina ya upasuaji uliokusudia kutoa viuvimbe vinavyo ota kwenye kuta za mji wa mimba (uterus).

Je upasuaji huu ni mkubwa au ni mdogo?

Huu ni upasuaji mkuwa ambao unaweza kuchukua zaidi ya dakika 45. Na kuna baadhi wa wanawake wanaweza wakawa na viuvimbe vingi zaidi ya 10 hivyo mda wa upasuaji unategemea zaidi na uwingi wa viuvimbe ulivyonavyo.

Kuna aina ngapi ya upasuaji huu wa myomectomy?

Kuna aina mbili za upasuaji lakini lengo ni moja na changamoto zake zinafanana kwa asilimia kubwa.

Aina ya kwanza inaitwa Open myomectomy: Njia hii ya upasuaji ndio njia ambayo inatumika zaidi hapa Tanzania pamoja na nchi nyingi za Africa. Kinachofanyika, mgonjwa baada ya kupewa sindano ya ganzi/usingizi, daktari husika atafungua tumbo kwa vifaa maalum na kisha ataweza kuona na kuanza kutoa viuvimbe vinavyokusudiwa kutolewa (Angalia video iliyowekwa mwishoni). Faida ya njia hii inamwezesha daktari kuwa na uwezo wa kushika mji wa mimba na kutambua kama kuna uvimbe uliopo ndani kabisa (sub-mucosa) na kuweza kuutoa. Changamoto ya njia hii ni maumivu baada ya upasuaji yanakuwa makali zaidi ukilinganisha na aina ya pili, hivyo hii upelekea wagonjwa kukaa zaidi hospitali kutokana na kushindwa kuanza kutembea mapema na kusababisha kuchelewa kurudi kwa mingurumo ya tumbo (bowel sounds).

Aina ya pili ya upasuaji unaitwa laparoscopic Myomectomy: Njia hii ya upasuaji daktari husika anatumia matundu madogo anayoyaweka tumboni ili kuweza kupitishia vifaa vya kuweza kutolea viuvimbe (Angalia mwisho mifano ya picha). Changamoto ya njia hii, daktari hana uwezo wa kushika mji wa mimba ila anaweza kuona kile anachokifanya kwenye luninga (TV) iliyounganishwa na vifaa vya upasuaji. Laparascopic myomecyomy inaweza kufanywa na madaktari walio pata taaluma maalum ya matumizi ya vifaa vidogo. Faida ya njia hii, maumivu na maambukizi ya bakteria baada ya upasuaji ni madogo, mda wa kukaa hospitali ni mchache na mgonjwa anaweza kuanza kutembea mapema zaidi ukilinganisha na aina ya kwanza.

Nani anatakiwa kufanyiwa upasiaji huu na nani hapaswi kufanyiwa?

Upasuaji huu wanaweza kufanyiwa wanawake wenye mambo yafuatayo:

Kwa mwanamke mwenye:

    • kutokwa na damu kupitiliza
    • maumivu makali sana kipindi cha hedhi.
    • maumivu makali kipindi cha kushikiri tendo la ndoa.
    • Kutokwa na damu ukeni baada ya tendo la ndoa.
    • Ugumba (infertility) unaotokana na uvimbe.
    • Maumivu makali ya mda wote ya tumbo la chini (chronic pelvic pain)

Watu wafuatao hawapaswi kufanyiwa upasuaji huu:

    • Kama hauna maumivu yoyote ya tumbo la chini
    • Kama umeshamaliza kuzaa na uvimbe hauna dalili yoyote.
    • Kama hedhi zako zimeshasimama na uvimbe hauna dalili yoyote
    • Kama haupo kwenye nyakati za kubeba mimba na bado hujafikiria kubeba mimba.

Nini faida ya upasuaji huu?

Upasuaji huu unazo faida zifuatazo:

  • Kuondoa maumivu ya tumbo.
  • Kuwezesha mwanamke kupata mimba.
  • Kuwezesha mwanamke kupata siku zake kawaida (damu za hedhi kutoka kwa uchache na maumivu kiasi)

Nini hasara ya upasuaji huu?

Upasuaji huu unahasara zifuatazo:

  • Kupata kovu mahala ulipopasuliwa
  • Kushindwa kupata ujauzito kutokana na utando (adhesion) unaojitengeneza baada ya upasuaji.
  • Kupelekea kutolewa mji wa mimba kama utatokwa na damu nyingi iliyoshindikana kudhibitiwa wakati wa upasuaji.

Tahadhari gani za kuchukua kabla ya kufanyiwa upasuaji huu?

Tahadhari ambazo zinatakiwa kuchukuliwa kabla ya upasuaji:

  • Kwa upande wa mgonjwa: Mgonjwa anatakiwa..
    • Kutokuficha taarifa zozote za afya yake kwa daktari anayekuhudumia.
    • Kutoa historia yako ya dawa na vyakula kama kuna ambavyo vinakudhuru au laa
    • Unatakiwa kupunguza uzito wa mwili kama unauzito wa kupindukia kwani upasuaji wa watu wenye uzito mkubwa unakuwa na changamoto nyingi.
    • Kama kunadawa za mda mrefu unazotumia kama za shinikizo la damu, sukari na hata dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi hutakiwi kuacha.
  • Kwa upande wa daktari:
    • Daktari atachunguza maeneyo yafuatayo ya mwili:
      • Moyo pamoja na mishipa yake (cardio-vascular system)
      • Mapafu (respiratory system)
      • Damu (kuchunguzwa magonjwa mbali mbali na kuona uwingi wa damu).

Hitimisho:

Myomectomy ni upasuaji usio wa dharula, hivyo kabla hujafanyiwa upasuaji huu ni vyema upate maelezo ya kina kutoka kwa daktari wako. Kwa wamama ambao hedhi zao zimeshafika kikomo (MENOPAUSE) na bado wanapata maumivu kutokana na uvimbe kwenye mji wa mimba ni vyema ufanyiwe upasuaji wa kutoa mji wa mimba kuliko uvimbe peke yake kwani kwa kufanya hivyo utakuwa umepunguza pia nafasi ya kupata saratani katika mji wa mimba (endometrial cancer). Vile vile, ni vyema kujua kwamba kama upo katika umri wa kuzaa (reproductive age group) baada ya kufanyiwa upasuaji wa awali viuvimbe hivi vinaweza kuota tena.

LAPAROSCOPIC MYOMECTOMY
OPEN MYOMECTOMY
Share na Wengine

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Appointment

Make appointment here