Mtoto Kutanguliza Makalio (Breech Presentation)

UJAUZITO:

Ni hali ambayo mwanamke anaipitia wakati kiumbe kinakuwa ndani ya mfuko wa uzani. Kipindi hiki kinaambatana na mabadiliko ya mwili (physiological changes). Katika ukuaji wa mimba kutokana na nafasi mtoto aliyokuwa nayo ndani ya mji wa mimba huwa wanahali ya kuzunguka mara kwa mara na kusababisha kuwa na matokeo tofauti ya mikao ya watoto. Mikao ya watoto ndani ya mji wa mimba ipo aina nyingi ila ulio wa hatari zaidi ni ule ambao makalio yanakuwa yametangulia (breech presentation).

 

Tatizo hili la kutanguliza makalio kwa watoto linachukua asilimia 3-4% kwa wazazi wanaofika mda wa kujifungua. Pia asilimia kubwa zaidi inapatwa na tatizo hili kama mimba inakuwa haijakomaa. Hii inamaana kwamba walio hatarini zaidi ni wenye mimba zilizo chini ya wiki 34 kwani kipindi hiki watoto wanakuwa bado hawajageuka.

 

Sababu zinazopelekea kwa watoto kutanguliza makalio ni kama zifuatazo:

 

1.  Ufupi wa kitovu (short cord) na kitovu kuzunguka shingo ya mtoto (nuchal cord): tatizo hili linafananishwa na mtu kujitundika kwenye kitanzi ambapo huwezi ukafurukuta zaidi ya kuendelea kukaa katika mlalo mmoja na kupelekea makalio kutangulia. Huwa inatokea zaidi kama zalio pia lipo juu (fundal placenta)

2.   Maji kuwa mengi (polyhydramnious): yanaruhusu mtoto kuwa na uwezo wa kuzunguka sana (unstable lie).

3.  Maji kuwa kidogo (oligohydramnious): yanamfanya mtoto akose nafasi ya kuzunguka ambapo kuta za mji wa uzazi zinamshikilia mtoto katika mlalo mmoja ambao pia unaweza leta vilema vya viungo.

4.  Uvimbe kwenye kuta za mji wa mimba (myoma uteri): uvimbe huu unaweza punguza eneo la chumba cha mtoto na kusababisha mtoto asipate nafasi ya kugeuka mwishowe kuishia mlalo mmoja wa kutanguliza makalio.

5.  Kutangulia kwa kondo au zalio (praevia): zalio (placenta) linapaswa kujishikiza kwenye mji wa mimba mbali na shingo ya uzazi. Lakini pale inapotokea likajipandikiza kwenye shinyo ya uzazi (cervix) na kuifunika inapelekea kwa watoto kutanguliza makalio na tatizo hili njia ya kujifungulia ni kwa upasuaji hata kama mtoto ametanguliza kichwa.

6.    Vilema vya watoto (fetal anomalies): kwa asilimia kubwa hii inatokea kwa watoto wenye vichwa maji (hydrocephalus).

7.    Mapacha (twins): kutokana na uhaba wa chumba, watoto wanapokuwa wawili katika mji wa mimba wanashindwa kugeuka mara kwa mara na hii inapelekea kukaa katika mkao mmoja.

 

Matokeo ya mlalo huu (breech presentation) unapofikia zaidi ya wiki 37 wazazi wengi wanapangiwa kuzalishwa kwa njia ya upasuaji (caesarean section) kwani ndio njia salama kwa mama na mtoto. Kwa baadhi ya wajawazito, madaktari wanaweza kujaribu kuwageuza watoto (external cephalic version) kabla ya kupatwa na uchungu na kisha kuwaweka kwenye uchungu. Kwa bahati mbaya maeneo mengine wajawazito wanakuwa hawana taarifa za milalo ya watoto wao kwani mimba ikishafika zaidi ya wiki 36 huwa wanaambiwa wakasubirie uchungu nyumbani ambapo sio sahihi. Mara nyingi makalio ya watoto yanakuwa madogo kuliko kichwa hivyo wakati wa uchungu mtoto anaweza akapitisha makalio kiurahisi kwenye njia ya uzazi lakini kichwa kikagoma kupita na kupelekea maji kuingia kwenye njia ya hewa (aspiration pneumonia) na wakati mwingine kupoteza uhai. Hii ndio sababu kuu inayopelekea sisi madaktari kuchagua upasuaji kama njia salama ya kujifungua.

Hitimisho: kwa wajawazito wote ili kuweza kujifungua kwa njia ya kawaida ni vyema kujua mlalo wa mtoto wako kati ya wiki 36-38. Ni nyema pia kuendelea kwenda clinic mpaka mwisho wa ujauzito. Pale inapotokea kwamba unahitajika kufanyiwa upasuaji wa kuzaa kutokana na mlalo wa mtoto usio sahihi ni vyema kukubaliana na daktari wako ili kuepusha matatizo makubwa yanayoweza kutokea kwa mama na mtoto. Kinga ni bora kuliko tiba.

Share na Wengine

Appointment

Make appointment here